MUWASA imeanza kusam...
MUWASA imeanza kusambaza Maji Safi Musoma Vijijini
25 Sep, 2024
MUWASA imeanza kusambaza Maji Safi Musoma Vijijini

MUWASA YAENDELEA KUSAMBAZA MAJI YA BOMBA MUSOMA VIJIJINI

Mitambo iliyofungwa Bukanga, Musoma Mjini, kwa ajili ya kuzalisha maji kutoka Ziwa Victoria ina uwezo wa kuzalisha lita milioni 36 za maji kwa siku - haya ni maji mengi ukilinganisha na mahitaji ya maji ya kila siku ya Mji wa Musoma

Tenki kubwa lenye ujazo wa lita milioni tatu (lita 3m) za maji limejengwa Mlimani Bharima (angalia picha iliyoambatanishwa hapa) kwa ajili ya usambazaji wa maji ya bomba ndani na nje ya Mji wa Musoma.

Serikali imeipa MUWASA jukumu la kusambaza maji ya bomba kutoka Tenki la Bharima kwenda vijiji jirani na Mji wa Musoma, vikiwemo vijiji vya Musoma Vijijini na Butiama.

Kata ambazo zimepangwa kusambaziwa maji ya MUWASA ni nne, ambazo ni Kata ya Etaro (vijiji 3), Nyegina (vijiji 3), Nyakatende (vijiji 4) na Ifulifu (vijiji 3).

MUWASA wamefanikiwa kusambaza maji ya bomba kwenye baadhi ya vijiji vya Kata ya Etaro (vijiji vya Busamba, Etaro na Mmahare) na Nyegina (kijiji cha Mkirira). Usambazaji unaendelea.

Kazi ya kutandaza bomba kuu la maji kuelekea Nyegina Senta inafanyika wakati huu - angali picha zilizoambatanishwa hapa

Baadhi ya vijiji vya Kata nne zilizotajwa hapo juu, vimeanza kutumia maji ya bomba kutoka vyanzo vilivyojengwa na RUWASA, na BADEA (maji kutoka Mugango).

Vijiji vyote 68 vina miradi ya maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria.

Vijiji 53 kati ya 68 vimeanza kutumia maji ya bomba (77.94% ya vijiji vyote), na vingine miradi iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.

Kuna vijiji vinachimbiwa visima virefu vya maji, na kazi hiyo inaendelea vizuri ndani ya Kata ya Bugwema.

Kazi nzuri na kubwa ya usambazaji wa maji ya bomba vijijini inafanywa na RUWASA, MUWASA, na Serikali kwa kushirikiana na wadau, BADEA (bomba la maji la Mugango-Kiabakari-Butiama).