Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizara ya Maji amekutana na Watumishi wa MUWASA

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Wizara ya Maji, Bi. Christina Akyoo, amekutana na kufanya kikao cha watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) leo tarehe 27 Agosti, 2025 kwa lengo la kufahamiana, kujua maendeleo ya kiutumishi kwa sababu ndio eneo analolisimamia, pia kufahamu changamoto zinazowakabili na kutafuta ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayoathiri utendaji wao.
Katika kikao hicho, Bi. Akyoo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kuhakikisha huduma za maji na usafi wa mazingira zinaboreshwa kwa manufaa ya wananchi wa Musoma na maeneo yanayosimamiwa na MUWASA ikiwa ni pamoja na Kanda ya Tarime, Shirati na Mugumu.
Pia amewasisitiza watumishi wa MUWASA kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa umma ili kuepuka uwepo wa mashauri ya utovu wa nidhamu.
Aliongeza kuwa watumishi kuzingatia utaratibu wa mawasiliano ya ndani ya ofisi kwa kusisitiza kuwa suala la mawasiliano lifuate utaratibu wa kiutumishi kuanzia uongozi wa ngazi ya chini hadi kufika kwenye ngazi za juu za uongozi.
Bi. Akyoo aliwakumbusha watumishi wa MUWASA kuwa watunzaji wa siri za taasisi kwa kutokutoka taarifa ambazo hazistahili. Kila mtumishi anahimizwa kuwa mlinzi wa taarifa za taasisi ili kuepuka kuathiri usalama wa taasisi na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Bi. Akyoo alitoa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA Mhandisi Nicas Mugisha kwa kuendelea kuboresha masilahi ya watumishi, pia kwa utekelezaji mzuri wa mfumo wa tathmini ya utendaji kazi wa Mamlaka ambapo MUWASA imepata alama 98.5.
Kwenye kikao hicho Bi. Akyoo alisema, Wizara ya Maji itaendelea kushirikiana na MUWASA katika kutatua changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi.
Kwa upande wa, watumishi wa MUWASA walitoa shukrani kwa uongozi wa Wizara ya Maji na kuahidi utayari wao kushirikiana kwa pamoja ili kufanikisha kufikia malengo ya MUWASA kwa kila mtumishi kutimiza wajibu wake.
MUWASA KAZI INAENDELEA