MUWASA yatoa elimu ya huduma ya maji Rwamlimi

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) imetoa elimu ya huduma ya maji kwa wakaazi wa Kata ya Rwamlimi, katika Mkutano uliofanyika eneo la shule ya msingi Rwamlimi tarehe 17.07.2025
Elimu hiyo imetolewa na Maafisa wa MUWASA Bi. Chausiku Joseph Marwa Afisa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma akishirikiana na Mkuu wa Kanda wa eneo hilo ndugu Raphael Joseph.
Wakieleza mipango ya MUWASA katika kata hiyo wameeleza kuwa MUWASA inaendelea na Uboreshaji huduma eneo la Rwamlimi ili kuhakikisha maji yanapatikana kwa wateja wake muda wote.
Aidha ufafanuzi umetolewa kuhusiana na uhaba wa maji kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo Rwamlimi kuwa MUWASA kwa kushirikiana na Tanesco wanaendelea kutatua changamoto ya umeme inayoathiri uzalishaji wa maji.
Katika kutatua changamoto hiyo MUWASA itatoa ufumbuzi wa muda mfupi ambao utahusisha ufungaji wa vifaa vya kuhimili kucheza kwa umeme (Thrystors) kwenye chanzo chake cha maji kilichopo Bukanga, ambapo hadi kufika mwishoni mwa mwezi Julai tatizo litakuwa limetatuliwa kwa asilimia sabini na kwa upande wa utatuzi wa muda mrefu MUWASA itafunga vifaa vinavyoitwa “Automatic Voltage Regulators” kwenye chanzo cha Bukanga na kituo cha kusukuma maji cha Nyamiongo.
Kwa upande wa Tanesco wanatarajia kufunga mitambo ya kuimarisha na kuboresha upatikanaji umeme (Static Synchronous Compsator- STATCOM) ambao utaondoa tatizo la kucheza kwa umeme maeneo yote ya Mkoa wa Mara.
Mtendaji wa Kata ya Rwamlimi ndugu Egasa Mwasandube, pamoja na Mtendaji wa Mtaa wa Rwamlimi ndugu Fredrick Marwa kwa pamoja wameishukuru sana MUWASA kwa elimu iliyotolewa kwani imesaidia kujibu maswali mengi kutoka kwa wananchi na kuleta uelewa wa pamoja.